Biblia inashuhudia kuwa umuhimu wa watu unatofautiana
Maandiko matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na
jinsi walivyomuamini Mungu na kutenda makuu kwa ajili ya taifa lake.
Abrahamu alimuamini Mungu akawa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio lililomfanya apate
baraka
ya pekee ya kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18).
Yosefu,
mwana mpenzi wa Yakobo,
alikuwa mwaminifu hata akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa
(Mwa 50:20).
Musa
ndiye mkombozi
wa taifa la Mungu katika Agano la Kale: aliongoza Israeli kutoka [[utumwani Misri
akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai.
Maandiko ya Agano la Kale yanakiri, “Wala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa
Musa” (Kumb 34:10-12).
Waliofuata
ni Yoshua, Debora, Gideoni, Ruthu,
Samweli, wafalme Daudi
na Solomoni, manabii Eliya,
Isaya, Yeremia, Ezekieli na wengineo.
Mwishoni
Yesu Kristo akamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Ni mkuu kati ya uzao
wa wanawake” (Lk 7:24-28).
Elizabeti, mama wa Yohane, alijiona hastahili
kutembelewa na Bikira Maria, Mama wa Yesu, akamuita, “Mama wa Bwana wangu” (Lk
1:43).
Bikira
Maria si mtu wa ziada katika mpango wa
Mungu bali ni mshiriki mkuu wa ukombozi
wa binadamu. Maria amechangia wokovu kwa kukubali
mpango wote wa Mungu aliyetaka amzae Mwanae, amlee na kumfuata kiaminifu hadi
msalabani, aliposhiriki kumtoa kama sadaka ya kutuokoa. Msimamo wake ulikuwa
mmoja tu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk
1:38).
Tukichunguza
nafasi yake katika fumbo
hilo, tunaweza kukiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu (Lk 1:49), kwa
kuwa, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu” (Yoh 3:27).
Yale
yote ambayo Wakristo wengi wanayasadiki kuhusu Bikira Maria,
hakujipatia bali alijaliwa na Mwenyezi Mungu huku akiitikia kwa hiari
fumbo la mpango wake.
Utabiri kuhusu Bikira Maria
Biblia
inatupatia utabiri
uliotolewa na Mungu mwanzoni mwa historia kuhusu mwanamke atakayemshinda nyoka
wa kale (Shetani): “Nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke,
kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa chako” (Mwa 3:15). Juu ya
[[Eva wa kale, ambaye alidanganywa na kuangushwa na Shetani atende dhambi, imesemwa: “Adamu akamwita mkewe jina
lake Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio hai” (Mwa 3:20). Hata hivyo Adamu
na Eva wa kale wametuletea kifo (Rom 5:12). Mababu wa Kanisa wanamtazama Bikira Maria kama Eva mpya
aliyemshinda Ibilisi na kuwa mama wa wote walio hai. Yesu,
aliye Adamu mpya,
alipokuwa anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Mama yake awe Mama wa
waliokombolewa kwa kumkabidhi mwanafunzi,
tena yule aliyempenda zaidi. “Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama
mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Kleopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu
alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu,
alimwambia mama yake, “Mama, tazama, mwanao”. Kisha akamwambia yule mwanafunzi,
“Tazama, mama yako”. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani
kwake. (Yoh 19:26-27).
Utabiri
mwingine ulisema, “Tazama Bikira atachukua mimba,
atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita jina lake Emanueli,
yaani Mungu pamoja nasi” (Isa 7:14). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:34-35,
“Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno
hili, maana sijui mume?
Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake
Aliye juu
zitakufunika kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu,
Mwana wa Mungu”. “Imba, ee binti Sion, piga
kelele, ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana yu
katikati yako” (Sef 3:14-15). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:28: “Malaika
akaingia nyumbani mwake akamwambia, ‘Furahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana
yu pamoja nawe’”. “Umebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na
katika kila taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika. Imani
yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele” (Yudithi 14:7; 15:9). Dondoo hilo linalinganishwa na
Lk 1:42, “Akapaza sauti kwa nguvu akasema, ‘Umebarikiwa wewe kuliko wanawake
wote, na yeye utakayemzaa amebarikiwa’”.
Bikira
Maria ni fumbo la ajabu alilolifanya Mungu katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Jamaa yake Elizabeti
alimpongeza tena akiongozwa na Roho Mtakatifu, “Heri yako
wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwana” (Lk 1:45).
Hivyo
manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu walimuagua Maria kwa heshima.
Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale yalitimia katika Agano Jipya: ukombozi ulianza Bikira Maria
alipokubali kwa imani fumbo la umwilisho wa Mwana wa
Mungu. Bikira Maria hakuwa “chombo” tu kilichotumika bila ya kuelewa, bali
alikuwa mshiriki huru wa kazi ya ukombozi ya Mwanae, kwa kuwa alipopashwa
habari na malaika alikubali kwa hiari mpango wa Mungu akisema, “Mimi ni
mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonena” (Lk 1:38).
Bikira Maria katika maisha ya Yesu
Yesu,
kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu na kuwatii wazee wake: “Basi, akarudi
pamoja nao Nazareti, akawa anawatii” (Lk 2:51).
Ishara
ya kwanza kwenye maisha
ya hadhara ya Yesu iliongozwa na Bikira Maria katika arusi ya Kana ya Galilaya, akisukumwa na huruma
kwa wenye shida: kwa ombi lake Yesu aligeuza maji
kuwa divai, na wanafunzi wake wakamwamini. Yohane
alisimulia hivi, “Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya;
naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na
wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, ‘Hawana
divai’. Yesu akamwambia, ‘Mama tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia’.
Mamaye akawaambia watumishi, ‘Lo lote atakalowaambia, fanyeni’. Basi kulikuwako
huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya
kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia,
‘Jalizeni mabalasi maji’. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, ‘Sasa tekeni,
mkampelekee mkuu wa meza’. Wakapelekea. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji
yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale
walioyateka yale maj), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia,
‘Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana
ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa’. Mwanzo
huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu
wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. (Yoh 2:1-12).
Bikira
Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake kuu kabisa, kuliko kwa kumchukua Yesu
tumboni tu. Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya roho
kuliko ya mwili. “Basi, mtu mmoja akamwambia, ‘Mama yako na ndugu zako wako
nje, wataka kusema nawe’. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu aliyemwambia hivyo,
‘Mama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?’ Kisha akanyosha mkono wake
juu ya wanafunzi wake akasema, ‘Hawa ndio Mama yangu na ndugu zangu, maana
yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu
na dada yangu na mama yangu’” (Math 12:46-50). Vilevile, wakati wa utume
wake, alimsikia “mwanamke mmoja katika lile kundi la watu akisema, ‘Hongera kwa
mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha’. Yesu akamjibu, ‘Barabara, lakini heri
yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na kulishika’” (Mk 11:27-28).
Bikira Maria alivyoshiriki Mateso ya Yesu
Katika
kumfuata Mwanae Bikira Maria alitabiriwa wazi na mzee Simeoni
uchungu
kama upanga utakaopenya moyo
wake, “Tazama huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na
kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama upanga utauchoma
moyo wako” (Lk 2:34-35).
Bikira
Maria alishiriki kwanza mateso
ya ukimbizi
huko Misri kwa lengo la kumficha Mwanae asiuawe na Herode Mkuu, “Hivyo Yosefu aliamka akamchukua
mtoto pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka
Herode alipokufa” (Math 2:14-15).
Bikira
Maria alishuhudia hatua kwa hatua kuteswa kwa Yesu; wanafunzi walipokimbia au
kumtazama kwa mbali, yeye alikuwa karibu akaona vema kila teso lililompata
Mwanae. Kutokana na fungamano la upendo wa ajabu lililokuwepo
kati ya Yesu na Mamaye, alipoyashuhudia yote aliteseka sana katika moyo wake
safi, kiasi kwamba Bernardo
wa Klervoo akasema, “Msalaba wa Yesu uliwasulubisha wote wawili,
Yesu mwilini na Mama yake moyoni”. Uaguzi wa mzee Simeoni ulitimia hivyo.
Kadiri
ya mtume Paulo kuteseka ni kutimiliza yaliyopungua
katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, “Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa
mateso yangu hapa duniani nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika
mateso ya Kristo” (Kol 1:24). “... maana tukiyashiriki mateso yake Kristo,
tutaushiriki pia utukufu
wake” (Rom 8:17b).
Pale
msalabani Bikira Maria, kwa njia ya mtume Yohane alifanywa Mama wa wote wanaompenda
Mwanae; kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa
uzima, pale alituzaa sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na
kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini
Mwanae aliyeonekana ameshindwa.
Bikira Maria baada ya kifo cha Yesu
Bikira
Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, akilivutia zaidi Roho Mtakatifu kwa sala
yake. “Hao wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha,
na Maria Mama yake Yesu na ndugu zake” (Mdo 1:14).
Yesu
alisema, “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili,
lakini atakapokuja huyo Roho wa
ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yoh 16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu
heshima kwa Bikira Maria ilienea katika Kanisa lote tangu zamani kabisa kadiri
ya utabiri wake kuwa ataheshimiwa na vizazi vyote, “Kwa kuwa amemwangalia kwa
huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenye
heri” (Lk 1:48).
Dogma za Kanisa Katoliki kuhusu Bikira Maria
Kuna
mafundisho makuu manne kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima kila Mkatoliki
ayasadiki kutokana na ufunuo wa Mungu: 1. B. Maria mkingiwa
dhambi ya asili 2. B. Maria Mama wa Mungu 3. B. Maria Bikira daima
4. B. Maria kupalizwa
mbinguni mwili na roho
Mkingiwa Dhambi ya Asili
Malaika
alimsalimia Maria “umejaa neema” (Lk 1:28) maana ndiye tunda bora la ukombozi
ulioletwa na Yesu. Ni imani ya Wakatoliki kwamba kwa stahili za Mwanae
alikingiwa asirithi kwa wazazi dhambi ya asili na madonda yanayotokana nayo,
wala asitende dhambi maisha yake yote. Kwa maneno mengine, Bikira Maria tangu
atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili
za Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Ndiye aliyekombolewa kwa namna
bora kushinda viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata
moja. Mapokeo ya mashariki yanamuita “A
Panagia” = “Mtakatifu tu”. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854,
halafu mwaka 1858 Bikira Maria alijitambulisha kama Mkingiwa
kwa Bernadeta
Soubirous huko Lurdi (Ufaransa). Tena mwaka 1917
huko Fatima (Ureno)
aliwafunulia Lusia, Fransisko na Yasinta Marto moyo wake safi
usio na doa.
Mama wa Mungu
Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo
mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno
alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana
alitwaa ubinadamu katika Bikira Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana
yake Mungu Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi katika yote isipokuwa dhambi.
Ubinadamu wa Yesu unategemea Nafsi yake ya Kimungu: akisema,
‘Mimi’, ni kwa Nafsi yake hiyo. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli nawaambia, kabla Abrahamu
hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50). “Kama vile Baba
alivyo asili ya
uhai, ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26).
Mtume
Paulo akaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na
mwanamke” (Gal 4:4). Bikira Maria ni Mama wa Mungu kwanzia wakati huo: tangu
Bikira Maria alipojaliwa kumchukua mimba, kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu
ambaye kwa asili ni Mungu. Cheo hicho kimemuinua juu kuliko hata malaika.
“Malaika alimwambia, ‘Hicho kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa
Mungu’” (Lk 1:35).
Dogma
ilitangazwa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa Efeso uliomuita “Mzazi wa Mungu”,
ukisema Maria anastahili kuitwa hivyo kwa sababu Mwana wa milele wa Mungu,
ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa mja mzito
alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?”
(Lk 1:42-43). Ungamo hilo la Elizabeti likakamilishwa na Mtume Thoma aliyemuambia Yesu mfufuka: “Bwana
wangu na Mungu wangu!” (Yoh 20:28).
Bikira na Mama
Wakristo
na Waislamu wote wanakiri kuwa Yesu alitungwa bila
ya mchango wa mwanamume. La ajabu zaidi katika imani hiyo ni kwamba hata uzazi
wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali uliutakasa: ni Bikira daima. Ingawa akili
inasita, ni lazima kukiri na malaika, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk
1:38). Yosefu,
ingawa kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa.
Ni
imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi kuwa Mama wa Yesu anastahili kuitwa “Bikira
daima” kwa sababu alimchukua mimba akiwa bikira, akamzaa bila ya kupotewa na
ubikira, akabaki bikira hadi mwisho wa maisha yake. Hamu yake ya kuwa bikira
hata kisha kuchumbiwa inajitokeza katika jibu alilompa malaika aliyemtabiria
mimba: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” (Lk 1:35). Ni kielelezo cha
Wakristo ambao Mtume Paulo aliwaandikia: “Nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa
kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi” (2Kor 11:2),
“mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine” (1Kor 7:35).
Wanaosemwa
katika Injili “ndugu zake Yesu” si watoto wa Bikira
Maria, bali ndugu wa ukoo waliokuwa jirani sana na familia hiyo takatifu. Kama
Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, Yesu angekuwa amefanya kosa la
kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume Yohane alipomkabidhi
msalabani, “‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi
alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).
Katika
Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19):
Yakobo huyo alikuwa maarufu katika Kanisa
la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo
si mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose
na mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu.
“Walikuwepo pia wanawake waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome
na Maria mama wa akina Yakobo mdogo
na Yose” (Mk 15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria
wakiwa wengi hivyo, tujue kuwatofautisha kwenye Injili, ambazo zinamtaja Bikira
Maria kama “Mama wa Yesu”.
Kupalizwa Mbinguni mwili na roho
Baada
ya maisha haya ya duniani Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho,
ishara ya mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke
aliyevikwa jua, pia na mwezi
chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya
kichwa chake” (Ufu 12:1). Maneno ya shangilio lake yametimia: Mungu
“amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk
1:52).
Imani
hiyo ya mapokeo ya kale, yanavyoshuhudiwa na Mababu wa Kanisa, ilitangazwa rasmi
na Papa Pius XII kwa niaba ya maaskofu wote mwaka 1950.
Heshima za Liturujia
ya Kiroma kwa Maria
Kuna
ibada za Mama Bikira Maria zinazoadhimishwa katika liturujia ya Kiroma. Hapa
zimepangwa kulingana na heshima zinavyozidiana:
8
Desemba – Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili 1 Januari – Bikira Maria Mama
wa Mungu 25 Machi – Bikira Maria Kupashwa Habari 15 Agosti – Bikira Maria
Kupalizwa Mbinguni
31
Mei – Maamkio
ya Bikira Maria 8 Septemba – Kuzaliwa kwa Bikira Maria
Juni
– Moyo Safi
wa Maria 15 Septemba – Mama Yetu wa Huzuni 22 Agosti – Bikira Maria Malkia 7
Oktoba – Bikira Maria wa Rozari
21 Novemba – Bikira Maria Kutolewa Hekaluni
11
Februari – Bikira Maria wa Lurdi 13 Mei – Bikira Maria wa Fatima 16 Julai –
Bikira Maria wa Mlima Karmeli
5 Agosti – Kutabaruku Kanisa la Bikira Maria 12 Septemba – Jina takatifu la
Maria 12 Desemba – Bikira Maria wa Guadalupe
Tena
kila Jumamosi isiyo na adhimisho maalumu, Kanisa
huadhimisha kumbukumbu ya Mama wa Mungu.
Pia
zipo heshima za binafsi kwa Bikira Maria: mashariki zinatumika tenzi na nyimbo
mbalimbali, k.mf. Akatistos
inayomuita “daraja linalounganisha dunia
na mbingu”, “ngazi
aliyoiona Yakobo” “kina kisichochunguzika kwa macho ya malaika” (Mwa 28:12);
magharibi]] anaheshimiwa kwa rozari.
Wakristo
wanaomheshimu Bikira Maria hawamuabudu hata kidogo, lakini wanamtolea heshima
ya juu kuliko watakatifu wengine. Tofauti ni kwamba Mungu tu anastahili
kuabudiwa (kwa Kigiriki, ‘latria’) watakatifu wanapewa heshima
(‘dulia’) na Bikira Maria heshima zaidi (‘yuper-dulia’). Kanisa Katoliki
linakiri neema zote za Mungu zinampitia Maria.
Bikira Maria kati ya Waorthodoksi
Kwa
kiasi kikubwa imani ya Waorthodoksi kuhusu Maria inalingana na ile ya
Wakatoliki, ingawa hawakubali jinsi baadhi ya dogma hizo zilivyotangazwa na jinsi
zinavyofafanuliwa.
Bikira Maria katika Uprotestanti
Martin Luther alipoanza Matengenezo ya
Kiprotestanti aliandika kwa heshima juu ya Bikira Maria, lakini
kadiri mabishano yalivyozidi kati ya madhehebu ya Kikristo, Waprotestanti walizidi
kupinga mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya Mama wa Yesu. Siku hizi baadhi
yake, hasa Waanglikana na Wamethodisti wanamrudishia Maria nafasi yake kama
kielelezo cha imani na cha kupokea neema ya Mungu.
Bikira Mariamu katika Uislamu
Kurani inamtaja mwanamke mmoja tu, tena mara 34: ni Mariamu,
mama wa nabii Isa. Akichanganywa na dada wa Haruni na Musa, aliyekuwa na jina hilohilo, anatajwa kama
binti Imrani.
Pia habari nyingine kadhaa zinapishana na zile za Injili.
Hata
hivyo anapewa heshima ya pekee, kama inavyoonekana katika sura ya 3:43: “Na
kumbukeni malaika waliposema, ‘Ewe Mariamu, kwa hakika Mwenyezi Mungu
amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa walimwengu”. Tena
katika aya 3:46: “Na kumbukeni waliposema malaika: ‘Ewe Mariamu, bila shaka
Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za Neno litokalo kwake, jina lake Masihi
Isa mwana wa Mariamu, mwenye heshima katika dunia na ahera, na yu miongoni mwa
waliokaribishwa’”.
Aliambiwa
amefanywa “ishara” pamoja na mwanae, ingawa haisemwi ni ishara ya nini. Sura ya
19, yenye jina lake, inaeleza kwamba Malaika Jibrili (Gabrieli) akimpasha
habari ya mimba alisema, ‘Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana
mtakatifu’. Akasema, ‘Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote,
wala mimi si mwasherati?’ Akasema, ‘Ni kama hivyo; Mola wako amesema: Haya ni
rahisi kwangu, na ili tukufanya ishara kwa mwanadamu na rehema itokayo kwetu,
na ni jambo lililokwisha hukumiwa’ ” (19:19-21). “Na mwanamke yule aliyejilinda
tupu yake na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe ishara kwa
walimwengu” (21:91).
Pamoja
na kusifiwa kwa usafi wake, anaongezewa sifa za imani na unyenyekevu: “Na
Mariamu binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo Roho yetu na
kayasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa
wanyenyekevu” (66:12).