KWARESMA
KUFUNGA KWARESMA
Nini maana ya Kwaresima?
Kwa Kilatini na Kiitaliano neno Kwaresima
lilimaanisha “40” yaani siku 40 za kufunga za wiki kati ya Jumatano ya Majivu
hadi Jumamosi Kuu. Kwa Kijerumani Kwaresima maana yake “Kipindi cha kufunga.”
Kwaresima ilianzaje?
Kabla ya kuona Kwaresima jinsi ilivyoanza, ni
vizuri kuongea kidogo kuhusu Sikukuu ya Pasaka ili tuweze kupata mwanga wa
kuelewa mwanzo wa kipindi hiki muhimu cha Kwaresima.
Habari Njema yatuambia kwamba YESU KRISTO
alifufuka “Siku ya kwanza ya juma.” “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku
ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda
kulitazama kaburi.” (Mt.28:1) Hii ni kwasababu Wakristo walianza kukutana
pamoja kwa sikukuu ya ufufuko wa BWANA kila wiki sio Jumamosi kama Wayahudi,
bali siku iliyo fuata. “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili
kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye
akafuliza -`maneno yake hata usiku wa manane.” (Mdo.20:7). “Siku ya Kwanza ya
juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake: ili
kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.” (1Kor.16:2), siku ambayo Warumi
waliita “Siku ya Jua”. Mara moja jina hilo lilibadilika na kuwa “Siku ya BWANA”
Kanisa la mwanzoni halikusherehekea sikukuu
kama vile Noel, Sikukuu kwa heshima ya Mama Bikira Maria au sikukuu yeyote ile.
Kulikuwepo na adhimisho la ufufuko wa BWANA kila wiki na hakuna zaidi.
Miaka mingi ikapita kanisa likiwa katika hali
hii. Baadaye kulikuwepo na hitaji la kusherehekea tukio la kiini cha imani yetu
kwa namna ya pekee. Wakristo waliona umuhimu wa kuwa na muda kwa sikukuu ya
kwanza kati ya sikukuu zao yaani “Jumapili ya Pasaka”, ambayo ilifikiriwa kama
“Mama wa Jumapili zote”, “Mama wa skikukuu zote”. Waliiona sikukuu hiyo kama
“Malkia wa sikukuu zote, wa Jumapili zote, na kiujumla kama Malkia wa siku zote
za mwaka. Tangu mwanzoni mwa karne ya pili, Jumuiya zote za Kikristo walikuwa
wanasherehekea sikukuu hii ya Pasaka. Sherehe zilikuwa zinahitimishwa na
kusanyiko la sala lililofanyika usiku na kumalizikia na Ekaristi. Ushiriki wa
kwenye ibada hiyo, ulichukuliwa kama ni kitu muhimu sana kwa mkristo.
Kuanza kwa Kwaresima.
Wote tunafahamu kwamba, ufanisi au mafanikio
yoyote ya sikukuu au ya jambo lolote yanategemea sana maandalizi yake. Miaka
miambili hivi baada ya KRISTO, Wakristo walitaka kuvuna matunda ya kiroho ya
Paska kwa wingi. Ili kufanikisha hili, walianzisha utamaduni wa kuwa na siku
tatu kabla ya Pasaka kwa sala, tafakari na kufunga kwa nia ya kuonyesha
masikitiko yao juu ya kifo cha YESU KRISTO. Kutokana na ukubwa na umuhimu wa
sikukuu hii, mbali ya kuona umuhimu wa maandalizi, walitafuta njia za kuongeza
muda wa furaha na utajiri wa kiroho utokanao na Pasaka. Hivyo walianzisha “Wiki
Saba,” yaani siku 50 za Pentekoste ambapo walisherehekea na kuzipitisha siku
hizo kwa hali ya furaha. Askofu Mt. Ireneus alisema kuwa muda huo wa siku 50 ni
kama Sikukuu ya Siku moja yenye umuhimu sawa na Jumapili. Katika kipindi cha
siku za Pentekoste, sala zilikuwa zinasaliwa hali wamesimama, kufunga
kulikatazwa na sakramenti ya ubatizo ilikuwa ikiadhimishwa. Ni kama vile
sikukuu ya Pasaka ilidumu kwa kipindi chote cha siku 50. Miaka 150 ilipita na
mwishoni mwa mwaka 350 B.K., Wakristo waliona kama siku tatu hazikutosha kwa
maandalizi ya sikukuu kama hii. Hivyo waliongeza hadi kufikia siku 40. Hivi
ndivyo Kwaresima ilivyoanza.
Kwa nini siku 40?
Tunaposema kuku wanne au kilo saba za mchele
tuna maana kama ilivyo yaani kuku wanne na kilo saba za mchele. Si zaidi au
pungufu.
Namba au tarakimu mbalimbali tunazokutana nazo
katika Biblia zinaashiria lugha za picha na siyo kuchukulia katika thamani ya
kuhesabu. Hivyio basi, tunapokutana na namba kama 40 huenda isimaanishe 40 kama
tunavyo hesabu fedha. Kati ya maana nyingi zilizotolewa kwa namba 40, kuna moja
yenye maana ya pekee, inamaana ya kipindi cha maandalizi cha kutosha
kisichokuwa na muda maalum, kwa tukio kubwa. Kwa mfano , Gharika ilidumu kwa
siku 40 usiku na mchana…na ilikuwa ni maandalizi ya ubinadamu mpya; Waisraeli
walitumia muda wa miaka 40 jangwani…maandalizi ya kuingia nchi ya ahadi; watu
wa Ninawi walifunga na kufanya kitubio siku 40…maandalizi ya kupokea msamaha wa
MUNGU; Elia alitembea kwa siku 40 mchana na usiku…kama maandalizi ya kufika
mlima wa MUNGU; Musa na YESU walifunga kwa siku 40 mchana na usiku… kama
maandalizi kabla ya kuanza utume wao. “Kisha ROHO alimwongoza YESU mpaka
jangwani ili ajaribiwe na ibilisi. Akafunga siku arobaini usiku na mchana, na
mwishoe akaona njaa” (Mt.4: 1-4)
Natumaini hadi hapo tumeelewa nini maana ya
namba 40. Je, ni siku ngapi ambazo zinahitajika kwa ajili ya maandalizi ya
sikukuu kubwa kuliko zote za kikristo? Bila shaka ni 40. (Kuanzia Jumatano ya
majivu hadi Jumamosi Kuu ukiondoa Jumapili zote) Siku 40 ni muda wa kutosha wa
kufanikisha kitu fulani chema, kizuri na chenye thamani.
Lengo la Kwaresima ni nini?
Lengo kuu la Kwaresima ni kufanya upya maisha
yetu ya kiroho na kutufanya kuwa watu ambao MUNGU anataka tuwe yaani ni kipindi
chenye kutupatia utakatifu, tukikumbuka kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu kama
BABA yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu (Mt. 5:48). Ni kipindi cha kuuvua utu
wetu wa kale na kuvaa utu mpya. Kwani tunasoma:- “Mvue kwa habari ya mwenendo
wa kwanza utu wa zamani, unao haribika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na
mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa na MUNGU
katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na
jirani yake…Mwibaji asiibe tena…Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu,
bali lililo jema na kufaa…tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma,
mkasameheane kama MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.” (Efe.4:22-32.)
Kwaresima kwa hakika ni kipindi pia cha
kuachana na matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya:
uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu,
hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na
hayo;” (Gal.5:19 – 20)
Kwa ufupi Kwaresima ni kipindi cha kuachana
na maisha ya dhambi na kurudi kwa MUNGU kwa kuishi maisha yanayompendeza MUNGU
kwa njia ya kufanya toba ya kweli isiyo ya mazoea, na malipizi yasiyo ya nje
tu, bali hasa mapinduzi ya kiroho. Katika kipindi hiki tunalazima ya kubadili
hali yetu ya ndani. Badala ya kujitafuta wenyewe na kufuata mapenzi yetu,
inatupasa sisi kumwelekea MUNGU na kuyatimiza mapenzi yake katika mawazo,
maneno na matendo yetu.
Nguzo tatu kuu za Kwaresima ni:-
i. Sala.
“Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha
ndani. Usali mbele ya BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini
atakujazi.” (Mt. 6:6)
Kupata muda wa sala pamoja na MUNGU. Sio tu
kunena maneno ya sala fulani, lakini pia kumsikiliza MUNGU akizungumza mioyoni
mwetu. Kumuomba MUNGU nguvu ya kubadilika, yaani uongofu wa kweli. Ndiyo maana
tunaambiwa. “Tubuni na kuiamini Injili”. Hayo ndiyo MUNGU aombayo kwetu wakati
wa Kwaresima. MUNGU anatuita kutoka kwa dhambi, na tuupokee ujumbe wake kwetu –
Injili, na kuwa waamninfu kuishi kadiri ya Injili. Ni wakati pia wa kuhudhuria
misa mara kwa mara kwa ibada na uchaji, kuhudhuria ibada mbalimbali, kama vile
Baraka ya Sakramenti Kuu, Kuabudu Ekaristi Takatifu, kusoma Neno la MUNGU na
kuliishi baada ya kuyatafakari maneno hayo ya MUNGU ambayo ndiyo sauti yake
MUNGU na kutumia muda wetu kwa mambo ya ki-MUNGU yaliyo matakatifu.
ii. Kufunga.
“Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani,
unawe uso wako ili usionekane na watu ukifunga, ila na BABA yako aliye sirini;
na BABA yako aonaye sirini atakutuza.” (Mt. 6:17-18). Kufunga sio tu kujinyima
kutokunywa pombe, kutokula chakula, kutovuta sigara n.k. Kifupi ni kwamba
kufunga kuondokana na ubinafsi wetu na kuwafikiria na kuwasaidia wenye shida.
Uovu hauwezi kushindwa bila kujitoa nafsi na bila kutoa na kuwapa wahitaji vile
tuvipendavyo. MUNGU hapendezwi na kufunga tu, bali upendo kwa wanaoteseka
utusukume na kufunga tupendavyo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Hivyo kuna
mahusiano makubwa sana kati ya kufunga na ukarimu. Kufunga lazima kuendane na
ukarimu. Kufunga bila ukarimu huo ni mfungo tasa.
iii. Kutoa Sadaka.
“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu
kusudi mtazamwe nao. Bali wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue
ufanyalo mkono wa kuume; na BABA yako aonaye kwa siri atakujazi.” (Mt. 6:1)
Hayo yanamaanisha kwamba usidai shukurani wala malipo kwa wema wowote
uwatendeao jirani zako kwa sadaka yako. Malipo utakayopata uyatazamie tu kutoka
kwa BABA yako wa mbinguni. Kutoa tunachojinyima kwa kumsaidia KRISTO anayeteseka
kwa wenzetu. Kushirikiana na wengine tulivyo navyo kama vile fedha, nguo,
chakula, ama kuwakaribisha wahitaji nyumbani.
Hivyo basi, Mazoezi tunayofanya katika
kipindi cha Kwaresima kama kusali zaidi, kusikiliza au kusoma Neno la MUNGU,
kutenda matendo ya huruma kwa wahitaji, kufunga chakula na kujihinisha kinywaji
pamoja na kuzuia tamaa potovu za mwili wetu, yawe na kusudi la kuibadili hali
yetu, kutufanya kuwa na upendo zaidi na huruma kwa wenzetu na kutufanya tuweze
kuunganika zaidi na KRISTO MFUFUKA. Tumvue mtu wa zamani katika nafsi zetu na
tumvae mtu mpya, yaani KRISTO Mfufuka.
Nini makusudi ya kufunga?
YESU alifunga ili awape wanadamu mfano au
kielelezo halisi na sahihi cha kuiga, na apate kuokoa roho zetu. Watu wawe na
namna bora ya kufanya malipizi, kuuadibisha na kuutumikisha mwili na tamaa kwa
kuwa anatenda dhambi.
Nani anapaswa kufunga?
Inatubidi tujiangalie sana kwani miili yetu
ni midhaifu na myepesi kwa kutenda dhambi na kuipeleka roho motoni.
Tusiiendekeze miili yetu, bali tuitawale kwa kufuata maadili ya kimungu na
kuinyima madai yake, ambayo ni kishawishi kinachotupeleka upotevuni. Tunapoamua
kufuata njia hii, hakika, KRISTO atatuimarisha na kutuongoza kwenye uzima wa
milele; na kutupa neema ya kupambanua mema na dhambi, huku tukielekea uzimani.
Mdomo unao nena dhambi, na mwili unaotenda dhambi, sherti vyote vitende pia
mema, siyo dhambi.
Mtu asiyetenda dhambi hana haja ya kufunga.
Lakini hakuna mtu anyefikia utu uzima ambaye hatendi dhambi machoni pa MUNGU
hata Wacha MUNGU wana dosari. Kwa hiyo, kila mtu afunge kufidia dhambi zake.
Tusipofunga kuna hatari kubwa ya kuungua moto. Ni vizuri waamini wote wafunge
ili kulipia fidia ya dhambi zinazotendwa. Tumwabudu KRISTO kwa unyofu na
unyenyekevu, ili kwa huruma yake kuu atusamehe dhambi zetu na adhabu
tunazostahili.
Ngazi tatu za kufunga chakula:-
(a) Ngazi ya kwanza, ni kuacha chakula kimoja fulani, au kitu kingine unachopendelea.
Kufunga huku ni rahisi hata kwa watoto. Kwa mfano, kuacha kula nyama au kunywa
soda yoyote kwa kipindi kizima cha Kwaresima; au kula chakula bila chumvi, au
kunywa chai bila sukari kwa kipindi kizima cha mfungo. Huu ni mfungo rahisi.
(b) Ngazi ya pili, ni kuacha kabisa kula siku nzima. Hii ni ngazi ya kawaida, yaani
mfungo wa kawaida. Huku ni kula mlo mmoja tu kwa siku hadi utosheke. Yawezekana
ikawa ukala mlo wa mchana au wa jioni tu. Asubuhi au jioni (au asubuhi na
mchana) ule kidogo sana. Katikati ya hapo usile chochote tena wala kunywa
chochote.
(c) Ngazi hii ya tatu, ni ya wale wanaotaka kufanya malipizi makali zaidi. Huu ni
Mfungo mkali. Katika ngazi hii ya kufunga watu wengi huaacha kabisa kula na
kunywa siku nzima, wakawa na huo mlo mmoja tu. Wanaotaka malipizi makali zaidi
siku ya kufunga chakula, asubuhi pokea Ekaristi Takatifu, na wala usiguse
chakula au kinywaji chochote kingine. Mchana unaweza kula slesi moja (kipande)
tu ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji ya kawaida. Jioni pia ule slesi moja
ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji. Na endapo utaamua kutokula kabisa na
kutokunywa kabisa hadi asubuhi kesho yake, itampendeza zaidi Mwenyezi MUNGU.
Hii ndiyo toba ya kweli.
Tukumbuke kwamba kile tunachofunga kiwasaidie
wasiojiweza. Si kufunga kwa nia ya kuweka akiba ili baada ya mfungo uweze
kutumia wewe mwenyewe! La hasha. Huo si mfungo wenye kuleta faida kiroho, bali
ni mfungo tasa.
Kuacha kula nyama Ijumaa Kuu na Ijumaa
nyingine za mwaka.
Ufungapo au uachapo kula nyama, funga kweli
na acha kweli kula nyama kwa dhati kwa toba ya dhambi. Vinginevyo utakuwa
unajidanganya mwenyewe. Papo uutolee mfungo wako na kutokula nyama huku kwa
Mwenyezi MUNGU, kwamba unafanya hivyo kwa kudhamiria. La sivyo utadhania
unafunga na unaacha kula nyama kwa manufaa ya kiroho wakati unashinda tu na
njaa ! Kuacha kula nyama maana yake ni kula vyakula vitokanavyo na ardhi tu;
ndivyo vyakula vya mfungo. Acha kula kila aina ya nyama, na mafuta yanayotokana
na wanyama. Usile nyama, mayai, mafuta ya wanyama, siagi na jibini, wala
maziwa. Kula vitu vyovyote vitokanavyo na wanyama au ndege hurahishisha mfungo
wako. Kumbuka pia kwamba siku za kufunga na kuacha kula nyama, uwe macho sana,
maana shetani mshawishi atakuja kupima utashi wako. Shinda mwili (njaa na kiu)
wako, mshinde shetani anyekuongoza dhambini. Jambo la muhimu hasa ni kwamba
matendo hayo yote yatendeke kwa ajili ya BWANA. Tuyafanye kama alama ya kwamba
tunataka kurudi kwake. Yawe ni matendo kati ya MUNGU na mimi. Kwa sababu hiyo
lazima kulinda siri ya jambo lolote tutakalo tenda. “BABA yako aonaye sirini
atakujazi.”
Nini thamani na maana ya kujinyima jambo
fulani ambalo kimsingi ni zuri na inafaa kwa ajili ya afya ya mwili?
Thamani na maana ya kufunga tunaiona na
kupata mfano kwa YESU. Ni vema tukumbuke kwamba Kwaresima inatukumbusha siku 40
za mfungo wa BWANA wetu jangwani, alivyofanya kabla ya kuanza Utume wake
hadharani, (Mt. 4:1-2). Pia, kama Musa alivyofunga kwa siku 40 usiku na mchana
kabla ya kupokea zile Mbao za Sheria (Kut. 34:28). Eliya naye alifunga kabla ya
kukutana na BWANA katika Mlima Horeb (1 Wafal. 19:8), YESU vile vile kwa njia
ya sala na kufunga, akijitayarisha kwa ajili ya majukumu yaliyokuwa mbele yake,
alituonesha tangu mwanzo mapambano makali dhidi ya Shetani.
Hivyo basi, Maandiko Matakatifu na mafundisho
yote ya desturi za ukristo yanafundisha kuwa mfungo ni msaada mkubwa katika
kukwepa dhambi na vishawishi vinavyoweza kutupeleka katika dhambi yenyewe. Kwa kuwa
kila mmoja wetu anaelemewa na dhambi na mafuatano yake, kufunga kumependekezwa
kwetu kama njia ya kurudisha urafiki wetu na MUNGU. Hivi ndivyo alivyofanya
Ezra (8:21), walivyofanya watu wa Ninawi (Yona 3:9).
Je, unajua mfungo wa kweli ni upi?
Mfungo wa kweli kama YESU alivyorudia mahali
pengi, ni kufanya mapenzi ya Baba aliye Mbinguni, “na BABA yako aonaye sirini,
na atakujazi” (Mt. 6:18). Mfungo wa kweli unaelekezwa katika kula chakula cha
kweli; yaani “kufanya mapenzi ya MUNGU” (Yn. 4:34).
Hivyo basi, kama katika Kwaresima hii UMEAMUA
kweli kusali, basi funga; kama unafunga, onesha huruma; kama unataka maombi
yako yasikiwe, sikiliza maombi ya wengine. Endapo hufungi masikio yako kwa
wengine, unafungua masikio ya MUNGU kwa ajili yako.
Kwa hakika mfungo unaleta faida za kimwili,
lakini kwa Mkristo mfungo upo kwa ajili ya “Tiba” ya kuponya yale yote
yanayouzuia mwili kutekeleza utashi wa MUNGU. Pia kufunga ni njia ya kuonesha
“huzuni” (1 Sam 31:13; 1 Fal 21:27; Neh1:4); toba (1 Sam 7:6; Yoe 2:12; Dan 9:3-4)
au hali ya “unyofu katika maombi” (2 Nya 20:3-4; Ezra 8:23).
Mpenzi msomaji wa kijitabu hiki, nakutakia
Kwaresima njema na mfungo wenye heri na toba ya kweli mbele za MUNGU kwa kuleta
mabadiliko ya kweli katika maisha yetu ili kufungua mifereji ya neema na baraka
katika mtu binafsi, familia na Jumuiya. Tukumbuke kwamba dhambi huzuia baraka
na neema toka kwa MUNGU hata kurudisha nyuma maisha yetu ya kiroho na maendeleo
katika familia. Hivyo, katika kipindi hiki cha Kwaresima tukitumie kwa kufanya
toba ya kweli kimatendo ili kuondoa vikwazo vyote vinavyo zuia maendeleo yetu
kiroho na ya kifamilia kwa kuwa tayari kumegwa kuwa chakula kwa wengine kwa
njia ya ukarimu wetu. Tujitahidi katika kushiriki Ibada ya Njia ya Msalaba
ikichukuliwa katika mtazamo wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa MUNGU.
Kushiriki Sakramenti vema hasa Sakramenti ya upatanisho ili mfungo, na toba
yetu vipate kibali machoni pake MUNGU na kushiriki matakatifu.
MUNGU akubariki na kukulinda. Nakutakia kwaresima njema.
“Wakati umetimia na ufalme wa MUNGU
umekaribia, Tubuni na kuiamini Injili.” (Mk 1:16).
Makala hii Na Fr. Rochus Conrad Mkoba.
Editor: Isaack J. Rimisho
TUMSIFU YESU KRISTO, TUBUNI NA KUIAMINI
INJILI