CCCF HUDUMA YA KILA JUMATANO

SIKUKUU YA MTAKATIFU PAPA YOHANE PAUL WA II (22 OCTOBER)

Tarehe 22 oktoba sikukuu ya Papa Yohane Paulo II (kwa Kilatini: Ioannes Paulus PP. II; kwa Kiitalia: Giovanni Paolo II; kwa Kipolandi: Jan Paweł II; kwa Kiingereza: John Paul II) aliishi tangu tarehe 18 Mei 1920 hadi tarehe 2 Aprili 2005.
Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Karol Józef Wojtyła
Alikuwa papa wa 264 kuanzia 16 Oktoba 1978 hadi kifo chake akidumu katika huduma hiyo kirefu kuliko mapapa wengine wote, isipokuwa Mtume Petro na Papa Pius IX.
Alimfuata Papa Yohane Paulo I akiwa Papa wa kwanza asiye Mwitalia tangu miaka 455 iliyopita, wakati wa Mholanzi Papa Adrian VI (1522 - 1523), tena papa wa kwanza kutoka Polandi (na makabila yoyote ya Waslavi) katika historia yote ya Kanisa. Alifuatwa na Papa Benedikto XVI.
Wengi wanamhesabu kati ya watu walioathiri zaidi karne ya 20, hasa kwa sababu tangu mwanzo wa upapa wake alipambana na Ukomunisti uliotesa nchi yake asili na nyinginezo, akachangia kwa kiasi kikubwa kikomo chake na kusambaratika kwa Urusi.
Vilevile alilaumu ubepari wa nchi za magharibi na kudai haki katika jamii zote, akitetea hasa uhai wa binadamu na uhuru wa dini.
Upande wa dini, aliboresha uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya Ukristo pamoja na ule na dini mbalimbali, kuanzia Uyahudi.
Ziara zake 104 kati nchi 129 ulimwenguni kote, mbali na 146 nchini Italia na 317 katika parokia za Roma, zilikusanya mara nyingi umati mkubwa (hadi zaidi ya milioni 4 huko Manila, Ufilipino), na kumfanya asafiri kuliko jumla ya mapapa wote waliomtangulia, akiwa mmojawapo kati ya viongozi wa dunia waliosafiri zaidi.
Papa Wojtyła alitangaza wenye heri 1,340 na watakatifu 483, ili kuwapa Wakristo wa leo vielelezo mbalimbali kwa maisha yao ili walenge utakatifu walioitiwa na Mungu. Idadi hiyo ni kubwa kuliko ile ya waliotangazwa na jumla ya Mapapa wote waliomtangulia walau katika karne tano za mwisho.
Alikuwa anaongea lugha mbalimbali, zikiwemo za Kipolandi, Kiitalia, Kifaransa, Kijerumani, Kiingereza, Kihispania, Kireno, Kiukraina, Kirusi, Kikroati, Kiesperanto, Kilatini na Kigiriki cha kale. [18]
Yohane Paulo II ametangazwa na mwandamizi wake Papa Benedikto XVI kuwa mwenye heri tarehe 1 Mei 2011, halafu Papa Fransisko akamtangaza mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014.
Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Oktoba, kulingana na siku ya kuanza rasmi huduma yake ya Kipapa.
====================================================================
Pia ni  kumbukumbuu ya  Mt. Mose Mwetiopia, Mtawa (405)

Mose alizaliwa nchini Etiopia karne ya nne. Wakati wa utoto wake alichukuliwa akauzwa kuwa mtumwa nchini Misri, akawa mtu mkubwa na mwenye nguvu. Kwa sababu ya wizi akafukuzwa na bwana wake, akawa kiongozi wa kundi la watu wabaya na wezi waliowatisha watu wa vijijini. Hatujui jinsi alivyoongoka; tumeambiwa tu kwamba alienda kukaa katika monasteri ya Petra katika jangwa la Skete (Misri). Baada ya muda, siku moja alishambuliwa na wezi wane, lakini akafaulu kuwashinda, akawafunga kwa kamba, akawapeleka kanisani, akisema; “sina ruhusa ya kuwajeruhi; basi, nifanyaje na wajinga hawa?” Wale majambazi wakaachiliwa, na inasemekana kwamba waliongoka wakawa wamonaki.
Mose hakugeuka kuwa mtakatifu kwa ghafla. Safari moja, alikata tamaa kabisa kadiri alivyona hatafaulu kamwe kuishinda hasira yake iliyokuwa kali sana. Basi, alimwendea Mt. Isidori, abati wa monasteri ya Pelusio (Misri) ambaye tangu ujana wake alikuwa monaki.
Abate huyo akamtangulia Mose hadi juu ya monasteri. Ilikuwa saa ya macheo ya jua. Abate Isidori akaangalia mashariki akasema: “Tazama, pale tu giza linaufanyia mwanga nafasi. Basi, ni hivyo rohoni mwetu”. Ndivyo alivyoimarishwa Mose. Akarudia kazi yake nzito, huduma na sala. Mungu alimrekebisha sana. Askofu wa Aleksandria (Misri) aliposikia habari utakatifu wake, akaamua kumpadrisha. Mose akazidi kujulikana mahali pengi kwa ajili ya fadhili zake.
Siku moja, wakati wa Kwaresima, aliwakaribisha wageni waliokuwa wakiona njaa kweli. Ijulikane kwamba wakati ule, hasa katika monasteri, amri ya kufunga chakula ilikuwa kali sana, lakini hata hivyo Mose alianza kuwapikia wageni wake. Wamonaki wenzake walipotambua Mose alikuwa anafanya nini, wakamkasirikia wakisema: “Mose anavunja sheria; baadaye tukamkaripia sana! Lakini wakabadili nia yao wakikubali kwamba, japo Mose alikuwa ameivunja sheria ya wanadamu, hata hivyo, alikuwa ameitimiza ile ya Mungu.
Siku nyingine, aliitwa mkutanoni mwa wamonaki kwa ajili ya kumhukumu mmoja wao ambaye alikuwa ametenda dhambi kubwa. Mose akaenda kwa shingo upande akibeba pakacha lililojaa mchanga, nao ulikuwa unavuja poole pole. Mose akasema: Nimekuja, na dhambu zangu zinanitoka; nanyi mnaniambia nimhukumu mwenzangu”. Kamwe hakuisahau amri ya Mungu kwamba “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa”.
Akiwa mzee, Mose aliuawa na majambazi wa kiarabu, huenda katika mwaka 405. Aliacha nyumba ikiwa na wafuasi sabini ambao wote walidumua katiak sala na utakatifu wa maisha. Jinsi gani tofauti ilviyokuwa kubwa kati ya kundi hilo na lile aliloliongoza zamani kabla hajamfahamu Mungu!
Tarehe hiyo hiyo tunakumbuka pia sikukuu ya Mwenyeheri Yosefina Leruu (1794) Mtawa na mfiadini
Alizaliwa mjini Kambre (Ufaransa) mwaka 1747. Katika mwka 1770, aliweka nadhiri za utawa katika shirika la masista fukara wa mt. Klara wanaoishi maisha ya ndani.
Serikali ya Ufaransa ilipopinduliwa, watu waliokuwa wapinzani wa dini wakaanza kuitawala nchi. Basi, muda mfupi baadaye mnamo mwaka 1790, serikali ikatoa amri ya kuzifunga konveti zote za masista wasio walimu wala manesi. Hivyo, sista Yosefina akarudi nyumbani.
Lakini baada ya muda mfupi tu, akachoka kuishi nje ya utawa, akaomba kujiunga na shirika la masista walimu.
Akakubaliwa, akakaa muda mfupi, na ndipo masista wote wakakamatwa, wakatiwa gerezani.

Mwaka 1794 wote walihukumiwa kufa. Inasemekana kwamba sita Yosefina alipanda jukwaani kwa raha, na alikuwa akiimba nyimbo wakati alipokuwa anaongojea zamu yake ya kukatwa kichwa.