HISTORIA YA KARISMATIKI
KUZALIWA KWA UPYAISHO WA KIKARISMATIKI KATOLIKI
Patti Gallagher Mansfield alikuwepo katika ile wikiendi ambayo kwa sasa ni maarufu ya Dukweni, wakati ambapo kikundi kidogo cha wanachuo wa Kimarekani katika mafungo ya mwisho wa wiki walipokea kipindi maalum cha neema kilichosaidia kuachilia Upyaisho wa Kikarismatiki katika kanisa Katoliki la Roma katika miaka ya mwishoni mwa 1960. Hapa chini anaelezea kilichotokea.
Mara nyingi watu wananiuliza kama nilishawahi kuchoka kuhadithia kilichotokea katika Wikiendi ya Dukweni. Kamwe sijawahi kuchoka, kwa sababu ni hadithi ya kimapenzi – hadithi ya jibu la kipekee na la neema la Mungu kwa maombi ya watu fulani wa kawaida sana.
Katika kipindi cha masika cha mwaka 1966, maprofesa wawili wa chuo cha Dukweni walikuwa WAKIOMBA, WAKITAFUTA NA KUBISHA. Walikuwa wamejiahidi kuomba kila siku kwa miminiko kuu la Roho Mtakatifu katika maisha yao wakitumia Sikwensia ya Pentekoste. Katikati ya kipindi hiki cha maombi, marafiki zao kadhaa waliwapa vitabu viwili: Msalaba na Upanga (The Cross and the Switchblade) na Wananena kwa Lugha Nyingine (They Speak With Other Tongues). Vitabu vyote vinaelezea uzoefu wa Ubatizo katika Roho Mtakatifu. Hawa maprofesa wakatambua kuwa Ubatizo katika Roho Mtakatifu ndio hasa waliokuwa wakiutafuta.
Januari 1967, Wakatoliki wanne kutoka Dukweni walihudhuria kwa mara ya kwanza mkutano wa sala wa Kikarismatiki wa mchanganyiko wa madhehebu – mkutano wa Chapel Hill – nyumbani kwa bi Flo Dodge, Mpresbiteri aliyejazwa Roho Mtakatifu. Jambo la kuvutia zaidi, miezi michache kabla Wakatoliki hawa hawajaja, Bwana Alimuongoza bi Flo kusoma Isaya 48 ambapo Anatangaza kwamba Yu karibu kutenda ‘jambo jipya’. Kwa hakika, Mungu Alikuwa Yu karibu kutenda jambo jipya miongoni mwa Wakatoliki kama matokeo ya mkutano wa sala. Wale watu kutoka Dukweni walivutiwa na kile walichokishuhudia kule. Tarehe 20 Januari, wawili miongoni mwao wakarudi tena. Wakapokea Ubatizo katika Roho Mtakatifu na kuanza kudhihirisha vipawa vya kikarismatiki. Wakarudi nyumbani kuomba na wale wengine wawili ambao hawakuhudhuria usiku ule.
Kipindi hiki nilikuwa ni mwanachama wa kikundi cha kusoma Maandiko cha Chi Rho kilichokuwa kikikutana pale chuoni Dukweni. Wawili kati ya hawa maprofesa walikuwa ni wasimamizi wa kikundi hiki, na ingawa hawakutuambia moja kwa moja juu ya uzoefu wao wa Kikarismatiki, wale waliowajua vizuri walitambua wana mwako wa furaha mpya. Tulikuwa tunapanga mafungo yetu ya Februari na maprofesa wakapendekeza mada mpya: “Roho Mtakatifu.” Katika maandalizi kwa ajili ya mafungo, walituambia tuombe kwa mategemeo/matarajio, tusome kitabu cha Msalaba na Upanga, na tusome sura nne za kwanza za kitabu cha Matendo ya Mitume.
Veni Creator Spiritus, “Njoo Roho Muumbaji”
Siku chache kabla ya mafungo, nilipiga magoti chumbani kwangu na kuomba,”Bwana, naamini nimekwisha kumpokea Roho Wako katika Ubatizo na Kipaimara. Lakini kama inawezekana kwa Roho Wako kutenda kazi zaidi maishani mwangu kuliko ambavyo amekuwa hadi sasa, NAMHITAJI!” Jibu kuu na la ajabu la maombi yangu lilikuwa li karibu kuja.
Tarehe 17 Februari watu 25 tuliondoka chuoni kwenda katika nyumba ya mafungo ya The Ark and The Dove (Safina na Njiwa) iliyokuwa nje kidogo ya jiji. Tulipokuwa tukikusanyika katika kila kipindi, maprofesa wetu walituambia tuimbe kama maombi tenzi ya zamani Veni Creator Spiritus, “Njoo Roho Muumbaji”. Ijumaa usiku kulikuwa na tafakari kwa Mama Maria. Kisha tukawa na Huduma ya Kitubio. Katika Injili ya Yohana tulisoma kwamba Roho Mtakatifu Atakapokuja Ataushuhudia Ulimwengu kwa habari ya dhambi. Hicho ndicho kilichotokea miongoni mwetu wakati tukitubu katika Sakramenti ya Upatanisho.
Jumamosi mshiriki mmoja wa kikundi cha sala cha Chapel Hill alikuja kuzungumza juu ya Matendo ya Mitume sura ya pili. Tulichoambiwa ni kwamba alikuwa ni rafiki wa Kiprotestanti wa maprofesa wetu. Ingawa uwasilishaji wake ulikuwa ni rahisi, ulijawa na nguvu za kiroho. Alizungumzia kujisalimisha kwa Yesu kama Bwana na Mkuu. Alimwelezea Roho Mtakatifu kama Nafsi Anayemtia nguvu kila siku. Huyu alikuwa mtu ambaye kwa hakika alionekana kumjua Yesu kwa undani na binafsi! Alijua nguvu za Roho Mtakatifu kama Mitume walivyojua. Nilijua nilitaka kile ambacho mtu huyu alikuwa nacho na niliandika katika notisi zangu, “Yesu, Uwe halisi kwangu.”
Katika majadiliano baada ya mafundisho yake, David Mangan akapendekeza kwamba tufunge mafungo yetu kwa kupyaisha Kipaimara chetu…kwamba sisi, kama vijana wakubwa, tuseme ‘ndiyo’ binafsi kwa Roho Mtakatifu. Niliunganisha mkono wangu na wake na kusema, “hata kama hakuna mwingine anayetaka kufanya hivi, ninafanya.” Kisha nilichana karatasi na kuandika, “Nataka muujiza!”, na kuibandika katika ubao wa matangazo.
Aina tofauti ya sherehe ya kuzaliwa
Jumamosi jioni ilikuwa imepangwa sherehe ya kuzaliwa kwa ajili ya wenzetu wachache, lakini hakuna aliyeonesha kujali ama kuvutiwa kikundini. Nilitembelea katika kanisa la orofani… si kwa ajili ya kuomba bali kumwambia mwanafunzi yoyote aliyekuwepo aje chini katika sherehe. Lakini, nilipoingia na kupiga magoti katika uwepo wa Yesu wa Ekaristi, nilitetemeka kwa hofu mbele ya Enzi Yake. Nilijua kwa jinsi isiyoelezeka kwamba Yeye ni Mfalme wa Wafalme, Bwana wa Mabwana. Nilifikiria, “Bora utoke hapa haraka kabla kitu hakijakutokea.” Lakini likishinda hofu yangu lilikuwa ni tamanio kuu zaidi la kujisalimisha bila masharti kwa Mungu.
Niliomba, “Baba, natoa maisha yangu kwako. Chochote Utakachoniambia, nakikubali. Na kama kikimaanisha mateso, nakikubali pia. Nifundishe tu kumfuata Yesu na kupenda kama Anavyopenda.” Katika muda uliofuata, nilijikuta nimelala kifudifudi, na nilifurikiwa na maonjo ya upendo wa huruma ya Mungu…upendo ambao kabisa haunistahili, lakini bado umetolewa bila kipimo. Ndiyo, ni kweli kile Mt. Paulo alichoandika, “Pendo la Mungu limemiminwa mioyoni mwetu na Roho mtakatifu.” Katika hali hiyo viatu vilinivuka. Kwa hakika nilikuwa katika ardhi takatifu. Nilihisi kama nilitaka kufa na kuwa na Mungu. Maombi ya Mt. Agustino yalinikaa: “O Bwana, umetuumba kwa ajili Yako na mioyo yetu haitotulia hadi pale imetulia katika Wewe.” Kadiri nilivyotaka kukaa uweponi Mwake, nilitambua kama mimi, nisie na upekee wowote, nimeweza kuonja Upendo wa Mungu kwa jinsi hii, basi yeyote katika uso wa dunia anaweza pia.
Nilikimbia chini kwa kiongozi wetu kumwambia kilichotokea na akaniambia kwamba David Mangan alikuwa kanisani kabla yangu na alikutana na Uwepo wa Mungu kwa jinsi hiyo hiyo. Wasichana wawili waliniambia kwamba uso wangu ulikuwa unawaka na wakataka kujua kilichotokea. Sikuwa naelewa sana maandiko kutambua ile sehemu katika Wakorintho wa Pili ambapo inamuelezea Musa ambaye uso wake ulikuwa unang’aa aliposhuka kutoka mlimani. Mt. Paulo anaandika, “Sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana tunabadilishwa kutoka utukufu hata utukufu.” Niliwaongoza hawa wanafunzi wawili katika kanisa na kuanza kuomba, “Bwana, kila ambacho umetoka kunifanyia, wafanyie!” Hiyo yamkini ilikuwa ndio Semina ya Maisha ya Kiroho fupi kuliko zote katika kumbukumbu!
Ndani ya saa lililofuata Mungu mwenyewe Aliwavuta wanafunzi wengi kanisani. Wengine walikuwa wanacheka, wengine wanalia. Wengine walikuwa wakiomba kwa lugha mpya, wengine (kama mimi) walihisi kama mikono inaungua. Mmoja wa maprofesa aliingia na kusema kwa mshangao, “Askofu atasemaje atakaposikia kwamba hawa watoto wote wamebatizwa katika Roho Mtakatifu!” Ndiyo, kulikuwa na sherehe ya kuzaliwa usiku ule, Mungu Alikuwa Ameipanga ifanyikie katika Kanisa la Chumba cha Juu. ILIKUWA NI KUZALIWA KWA UPYAISHO KARISMATIKI KATOLIKI!
“Sihitaji tena kuamini katika Pentekoste; Nimeiona!”
duquesne-weekend
Turiporudi chuo, tulileta vurugu kwelikweli. Rafiki mmoja aliniambia, “Patti, kama nisingekuwa nakujua vizuri, ningesema ulikuwa umelewa!” Kama Mitume baada ya Pentekoste, hatukuweza kujizuia tusiseme yale tuliyoyaona na kuyasikia. Tulijikwaa katika vipawa vya kikarismatiki kama unabii, kupambanua roho, na uponyaji. Mmoja wa maprofesa wetu alishuhudia kwa marafiki zake huko Notre Dame na chuo kikuu cha jimbo la Michigan kwa maneno haya: “Sihitaji tena kuamini katika Pentekoste; Nimeiona!” Katika miaka hii iliyopita neema ya hii Pentekoste Mpya imesambaa kutoka kwa wanafunzi wachache katika Wikiendi ya Dukweni hadi kwa mamilioni ya Wakatoliki duniani kote. Kwa nini? Kwa sababu Mungu Amekusudia kumtuma Roho Wake kufanya upya uso wa nchi! Nikirudia sala ya Mama Maria, nataka kutangaza kwamba, “Mungu Mwenye Nguvu Ametutendea makuu, na Jina Lake ni takatifu!”
Subscribe to:
Posts (Atom)