KUHUSU HII NOVENA YA HURUMA YA MUNGU
Hizi ni sala ambazo Bwana Yesu mwenyewe alimfundisha Mtakatifu Sista Faustina Kowalska. Bwana Yesu alimwambia: “Kwa Novena hii, nitazijaza roho za watu kila neema iwezekanavyo. Uisali daima rozari hii niliyokufundisha. Na yeyote atakayeisali Rozari hii atajaliwa kupata Huruma Kuu ya Mungu saa ya kufa kwake, hata wakosefu shupavu wakisali Rozari hii, hata kama ni mara moja tu, wataipata Huruma Yangu isiyo na mwisho. Kwa njia ya Rozari hii, unaweza kuomba chochote na utakipata, bora tu kipatane na mapenzi yangu. Ninataka dunia nzima iijue Huruma Yangu isiyo na mwisho. Nami ninataka kuwapa neema nyingi wale wanaoitukuza Huruma Yangu, hata neema zile wasizofikiria kuzipata”.
Kwa kila neno moja la Novena hii, tone moja la Damu Takatifu hutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu na kuidondokea roho moja ya mkosefu.
“Heri mtu Yule ambaye katika maisha yake amejizoeza kuikimbilia Huruma ya Mungu, kwa maana siku ya Hukumu ya Mwisho hatahukumiwa. Huruma ya Mungu itamkinga. Mwanangu, wahimize watu waisali hii Rozari ya Huruma niliyokufundisha. Kwa kusali Rozari hii nitawapa kila neema watakayoniomba. Hata wakosefu wagumu wakiisali nitajaza roho zao kwa amani, na nitawajalia kifo chema. Wanapoisali Rozari hii karibu na mtu anayekufa, mimi nitasimama katikati ya roho hiyo na Baba Yangu, si kama Hakimu mwenye Haki, bali kama Mwokozi mwenye Huruma”.
NAMNA YA KUFANYA NOVENA KWA HURUMA YA MUNGU
Anza Novena hii siku ya Ijumaa Kuu kwa siku tisa (unamaliza Novena kabla ya Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka, “Jumapili ya Huruma ya Mungu”). Lakini unaweza kufanya Novena hii wakati wowote mwakani, isipokuwa Novena ianzwe katika siku ya Ijumaa.
1. Uje Roho Mtakatifu:
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waumini wako, washa mapendo yako, peleka Roho wako, vitaumbwa upya na nchi zitageuka.
Tuombe; Ee Mungu uliyefundisha nyoyo za waumini wako, ukiwaletea mwanga wa Roho wako Mtakatifu, tunakuomba utuongoze na Yule Roho, tupende yaliyo mema, tupate daima faraja zake, tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu, Amina.
2. Sala ya kutubu:
Mungu wangu, ninatubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi, basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi kwako, Amina.
3. Weka nia ya sala za leo:
Kila siku ya Novena soma maneno ya Bwana Yesu kwa kuweka nia ya sala za siku hiyo, na pia Sali sala fupi kuhusu nia husika kama zilivyoonyeshwa hapo chini, kisha;
4. Tumia Rozari ya kawaida kusali Rozari ya Huruma ya Mungu kama ifuatavyo:
Baba yetu … Salamu Maria …. X3 Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi …….
Kila penye punje kubwa (Badala ya Baba yetu):
Baba wa Milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu, wa Mwanao Mpenzi sana, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zetu, na dhambi za dunia nzima.
Kila penye punje ndogo (badala ya Salamu Maria):
Mwanzishaji: Kwa ajili ya mateso makali ya Bwana wetu Yesu Kristu,
Wote huitika: Utuhurumie sisi na dunia nzima.
Mwisho wa Rozari sali mara tatu sala ifuatayo:
Mungu Mtakatifu, Mtakatifu mwenye Enzi, Mtakatifu unayeishi milele, Utuhurumie sisi na dunia nzima.
5. Litania ya Huruma ya Mungu
Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie
Kristu utuhurumie – Kristu utuhurumie
Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie
Kristu utusikie – Kristu utusikilize
Baba wa mbinguni Mungu – utuhurumie
Mwana Mkombozi wa dunia Mungu - utuhurumie
Roho Mtakatifu Mungu - utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu mmoja – utuhurumie.
Huruma ya Mungu iliyo sifa kuu ya Muumba wetu - Tunakutumainia (iwe kiitikio)
Huruma ya Mungu iliyo kilele cha ukamilifu wa Mwokozi wetu
Huruma ya Mungu iliyo upendo usiopimika wa Roho Mtakasa
Huruma ya Mungu fumbo lisilofahamika la Utatu Mtakatifu
Huruma ya Mungu iliyo ishara ya uwezo mkuu wa Mungu Mwenyezi
Huruma ya Mungu iliyofumbuliwa katika kuziumba Roho za Malaika wa mbinguni
Huruma ya Mungu iliyotuumba na kutuamuru tuwepo bila kutokana na chochote
Huruma ya Mungu inayotujalia maisha ya kutokufa
Huruma ya Mungu inayotukinga na adhabu tunazostahili
Huruma ya Mungu inayotuinua tutoke katika taabu, unyonge na maumivu ya dhambi zetu
Huruma ya Mungu inayotufanya wenye haki katika Neno aliyejifanya Mtu
Huruma ya Mungu inayofurika kutoka katika majeraha ya Kristu
Huruma ya Mungu inayobubujika kutoka ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
Huruma ya Mungu iliyotupatia Bikira Maria Mtukufu awe kwetu Mama wa Huruma
Huruma ya Mungu iliyoonyeshwa katika kuanzishwa Kanisa Katoliki
Huruma ya Mungu inayopatikana katika mafumbo ya Sakramenti Takatifu
Huruma ya Mungu inayotolewa kwa wanadamu wote kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kitubio
Huruma ya Mungu inayotolewa katika Sakramenti ya Ekaristi na Upadrisho
Huruma ya Mungu inayoonyeshwa kwetu pale inapotuita na kutuingiza katika kuwatakatifuza wenye haki
Huruma ya Mungu inayotimilika katika ukamilifu wa watu watakatifu
Huruma ya Mungu chemchemi ya afya kwa wagonjwa na wote wanaoteseka
Huruma ya Mungu iliyo faraja ya wote wenye uchungu moyoni
Huruma ya Mungu iliyo tumaini la roho zinazosumbuliwa na mkato wa tamaa
Huruma ya Mungu iliyo mwenzi wa daima na popote wa watu wote
Huruma ya Mungu inayowahi kutuletea neema zake
Huruma ya Mungu iliyo amani yao wanaokufa
Huruma ya Mungu iliyo burudisho na faraja yao marehemu wa toharani
Huruma ya Mungu iliyo furaha ya mbinguni kwa watakatifu wote
Huruma ya Mungu iliyo taji la watakatifu wote
Huruma ya Mungu chemchemi ya miujiza isiyokauka
Mwanakondoo wa Mungu uliyetuonyesha huruma yako kuu katika kuikomboa dunia kwa msalaba wako mtakatifu, - utusamehe ee Bwana
Mwanakondoo wa Mungu unayejitolea kwetu kwa mapendo na huruma katika kila adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu,- utusikilize ee Bwana
Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia kwa njia ya huruma yako isiyo na mwisho,- utuhurumie.
Kiongozi : Bwana utuhurumie –
Wote: Kristu utuhurumie, Bwana utuhurumie.
Kiongozi : Huruma anana za Bwana zi juu ya kazi zake zote –
Wote: Huruma za Bwana nitaziimba milele.
Tuombe: Ee Mungu uliye na huruma isiyo na mwisho, na hazina za wema na upendo wako hazina mipaka. Tunakusihi ututazame sisi watu wako huku duniani na kutuongezea huruma yako tena na tena, ili itusaidie tusije tukakata tamaa hata mara moja, haidhuru tukumbane na majaribu makubwa kiasi gani, bali tuweze daima kuzielekea na kuzishika amri zako, kwa matumaini na kutimiza mapenzi yako matakatifu, ambayo ndiyo huruma yenyewe. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu Mwanao, Mfalme wa Amani na Huruma, aishiye na kutawala nawe, na Roho Mtakatifu, kwa pamoja mkituonyesha huruma, daima na milele. Amina.
NIA ZA KILA SIKU WAKATI WA KUFANYA NOVENA YA HURUMA YA MUNGU
SIKU YA KWANZA
Maneno ya Bwana Yesu: “Leo niletee wanadamu wote kijumla, hasa wakosefu wote. Uwazamishe ndani ya Bahari Kuu ya Huruma yangu. Kwa njia hii utatuliza uchungu wangu kwa ajili ya roho zilizopotea.”
Kiongozi: Tuombe Huruma kwa ajili ya wanadamu wote, hasa kwa ajili ya wakosefu.
Wote: Ee Yesu mwenye Huruma kabisa, ambaye asili yako ni Huruma na Msamaha, usizitazame dhambi zetu, bali utazame tumaini tulilo nalo katika wema wako usio na mwisho. Utupokee sisi sote chini ya ulinzi wa Moyo wako wenye Huruma tele. Usimwache hata mmoja. Tunakuomba hayo kwa njia ya upendo ule unaokuunganisha wewe na Baba na Roho Mtakatifu, katika Umoja wa Utatu Mtakatifu, daima na milele. Amina.
Baba yetu …….. Salamu Maria ……... Atukuzwe …….…
Baba wa Milele, uwatazame kwa macho ya huruma wanadamu wote, na hasa wakosefu maskini, waliongizwa ndani ya Moyo wa Mwanao mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, ulio na huruma yako kuu, ili nasi tuisifu na kuitukuza tangu sasa na milele yote. Amina.
SIKU YA PILI
Maneno ya Mwokozi: “Leo niletee mapadri wote na watawa. Uwazamishe katika kilindi cha huruma yangu isiyo na mwisho. Ni wao hasa walionipa nguvu ya kuweza kuyavumilia mateso yangu makali mno. Kwa njia yao, kama vile mifereji, huruma yangu humiminika na kuwatiririkia wote.”
Kiongozi: Tuwaombee watawa wote wanawake ili wadumu kiaminifu katika utumishi wao na wakfu wa maisha yao kwa Yesu Kristu Bwanaharusi wao.”
Wote: Ee Yesu mwenye huruma tele, kwako hutoka mema yote. Uwazidishie neema yako watawa wanawake waliojitolea na kuwekwa wakfu katika utumishi wako, ili watekeleze utumishi wao kwa huruma na kwa jinsi inayofaa, na kwamba wale wanaowaona na kuzishuhudia kazi zao bora, waweze kumtukuza Baba wa Huruma aliye mbinguni. Amina.
Baba yetu ……. Salamu Maria …… Atukuzwe ……
Kiongozi: Tuwaombee mapadri na watawa wote ambao ni vyombo vya huruma ya Mungu.
Wote: Baba wa Milele, elekeza macho yako yenye huruma, juu ya jeshi teule la wafanyakazi shambani mwako. Uzitazame kwa wema roho zao mapadre na watawa wote. Uwajalie wingi wa Baraka zako. Kwa njia ya upendo wa Moyo wa Mwanao, humo ambamo wameingizwa, uwape nguvu na mwanga, ili waweze kuwaongoza wengine katika njia ya wokovu, na kwa sauti moja, waihimidi huruma yako kwa nyimbo za sifa bila mwisho. Amina.
SIKU YA TATU
Maneno ya Bwana Yesu: “Leo niletee roho za watu wenye uaminifu na uchaji wa Mungu, na uwazamishe katika Bahari Kuu ya Huruma yangu. Roho za watu hawa ndizo zilizonifariji katika njia ya Msalaba. Wao ndio waliokuwa tone lile la faraja nilipokuwa katikati ya bahari ya uchungu na mateso.”
Kiongozi: Tuwaombee watu wote waaminifu na wenye ibada ambao walimtuliza Yesu katika mateso yake.
Wote: Ee Yesu mpole na mwenye huruma sana, Wewe huchota neema kwa wingi kutoka katika hazina Yako, na kuzigawa kwa ukarimu kwa kila mmoja wetu na kwa watu wote. Tunakuomba utupokee katika makao ya Moyo wako mpole na wenye huruma nyingi, na usituache tutoroke humo kamwe. Tunakuomba neema hii, kwa ajili ya mapendo ya ajabu, yawakayo moyoni mwako kwa Baba yako wa mbinguni. Amina.
Baba yetu …….. Salamu Maria …….. Atukuzwe …….
Wote: Baba wa Milele, elekeza macho yako yenye huruma, kwa watu wote walio waaminifu, kama vile kwenye hazina na urithi wa Mwanao. Kwa ajili ya mateso yake ya kuhuzunisha, uwajalie Baraka zako, na ulinzi wako daima. Kwa njia hii, waweze kuimarika katika upendo, na wala wasije wakapoteza hazina bora ya Imani Tashi Takatifu, bali, pamoja na majeshi yote ya malaika na watakatifu, waweze kuisifu na kuitukuza huruma yako isiyo na mwisho, kwa milele yote. Amina.
SIKU YA NNE
Maneno ya Bwana Yesu: “Leo niletee wale wote wasioniamini na wale wasionijua bado. Wao pia niliwafikiria wakati wa mateso yangu makali, na juhudi watakayokuwa nayo baadaye ilinituliza Moyo wangu. Uwaingize katika Bahari Kuu ya Huruma Yangu.”
Kiongozi: Tuwaombee watu wote wasiomwamini Kristu, pamoja na wale wasiomjua bado.
Wote: Ee Yesu mwema, Wewe ni Mwanga wa dunia nzima, uzipokee katika makao ya Moyo wako wenye huruma sana, roho za wale wote wasiokuamini na wale wasiokujua bado. Achia mionzi ya neema yako iwaangazie, ili nao pia pamoja nasi sote. Waweze kuitukuza huruma yako ya ajabu, na usiwaache wakatoroka makao hayo, ambayo ni Moyo wako uliojaa huruma. Amina.
Baba yetu ……… Salamu Maria ……. Atukuzwe ………
Wote: Baba wa Milele, elekeza macho yako yenye huruma, kwa roho za watu wale wasiomwamini Mwanao, na za wale ambao hawajakujua Wewe bado, ambao tumewaingiza ndani ya Moyo wa Yesu uliojaa huruma tele. Uwavute kwenye mwanga wa Injili, watu hawa hawajui Ukuu wa furaha iliyopo katika kukupenda Wewe. Uwajalie nao pia waweze kuitukuza hisani ya huruma yako, kwa miaka isiyo na mwisho. Amina.
SIKU YA TANO
Maneno ya Mkombozi: “Leo niletee roho za ndugu waliojitenga na Kanisa, na uwazamishe katika Bahari Kuu ya Huruma yangu. Wakati ule wa mateso yangu makali, watu hawa waliurarua mwili wangu na roho yangu, yaani Kanisa langu. Pindi warudipo tena katika Umoja wa Kanisa, majeraha yangu hupona, na kwa njia hii wanapunguza ukali wa mateso yangu”.
Kiongozi: Tuwaombee wale waliopotoka katika Imani Katoliki na kujitenga na Kanisa.
Wote: Ee Yesu Mpole na mwenye Huruma, Wewe u Huruma na Wema wenyewe, hukatai kuwapa mwanga wale wote wanaoutafuta. Uzipokee ndani ya Moyo wako wenye Huruma, roho za ndugu zetu waliojitenga. Uwavute kwa mwanga wako, ili warudi tena katika Umoja wa Kanisa lako Takatifu, na uwadumishe humo, wasiweze kutoroka tena Moyo wako wenye Huruma sana, bali uwawezeshe wao pia pamoja nasi, kuusifu na kuutukuza ukarimu wa Huruma Yako Kuu, kwa milele na milele. Amina.
Baba yetu ……. Salamu Maria …….. Atukuzwe …………..
Wote: Baba wa Milele, uzielekee kwa macho ya huruma, roho za ndugu zetu waliojitenga na Kanisa lako Takatifu, hasa wale waliozitapanya Baraka zako na kuzitumia vibaya neema zako, kwa kuendelea kishupavu katika mafundisho yao ya upotofu. Usiyaangalie hayo makosa yao, bali uutazame upendo wa Mwanao Mpenzi, pamoja na mateso yake makali aliyovumilia kwa ajili yao. Watu hawa pia, wameingizwa ndani ya Moyo wa Yesu Mwanao, wenye Huruma Kuu. Uwawezeshe vile kwamba, wao pamoja na sisi sote, tuisifu na kuitukuza Huruma Yako Kuu, kwa milele na milele. Amina.
SIKU YA SITA
Maneno ya Mwokozi wetu: “Leo niletee roho za watu walio wapole na wanyenyekevu wa moyo, pamoja na roho za watoto wadogo, na uzizamishe katika kilindi cha Huruma yangu. Roho hizi hufanana kwa ukaribu zaidi na Moyo wangu. Watu hawa ndio walionitia nguvu wakati wa mateso na uchungu wa mahututi yangu. Niliwaona kama malaika wa duniani, ambao watakesha daima kuabudu katika altare zangu. Kwa mafuriko yangu, nitawamwagia neema zangu zote, kwa maana ni roho ile tu iliyo na unyenyekevu inaweza kupata neema zangu. Ninawapendelea watu walio wanyenyekevu na kuwaamini sana.”
Kiongozi: Tuwaombee watoto wadogo pamoja na roho zile zenye unyofu kama wao.
Wote: Ee Yesu mwenye Huruma sana, Wewe Mwenyewe ulisema: “Jifunzeni kwangu kwa maana Mimi ni mpole na mnyenyekevu wa Moyo”, uwapokee ndani ya Moyo wako uliojaa Huruma, watu wote walio wapole na wanyenyekevu, pamoja na roho za watoto wadogo. Roho hizi hustaajabisha Mbingu nzima, maana wanapotokea mbele ya Kiti cha Enzi cha Baba wa mbinguni, huwa kama shada la maua litoalo harufu tamu ya marhamu safi, na kuifurahisha Mbingu nzima. Mungu Mwenyewe hufurahia manukato yao safi. Roho hizi zina makao ya daima ndani ya Moyo wako wenye Huruma ee Yesu. Na daima hukuimbia wimbo wa Huruma na Upendo wako. Amina.
Baba yetu …… Salamu Maria …….. Atukuzwe …….
Wote: Baba wa Milele, uzitazame kwa macho ya Huruma, roho za watu wote walio wapole na wanyenyekevu wa moyo, pamoja na roho za watoto wadogo, walioingizwa katika makao ambayo ni Moyo wa Yesu Mpenzi, ulio na Huruma nyingi. Roho za watu hawa, hufanana na Mwanao kwa kwa karibu zaidi. Harufu yao tamu ya fadhila hukufurahisha sana, nayo hupanda ikianzia hapa duniani mpaka kwenye Kiti chako Kitukufu. Ee Baba wa Huruma na wema wote, ninakuomba, kwa ule upendo ulio nao kwa roho hizi penzi, na kwa ajili ya furaha uipatayo kwao, utubariki sisi na dunia nzima, ili sote pamoja tuungane katika kuisifu Huruma Yako, kwa milele yote. Amina.
SIKU YA SABA
Maneno ya Mwokozi: “Leo niletee roho za wale ambao kwa namna ya pekee huiheshimu na kuitukuza Huruma yangu, na uwazamishe ndani ya Huruma Yangu. Roho hizi ndizo zilizonisikitikia zaidi wakati wa mateso yangu na kuipenya kabisa roho yangu. Hawa ndio vielelezo na sura halisi ya Moyo wangu wenye Huruma na Wema. Roho hizi zitakuja kung’aa kwa namna ya pekee katika maisha ya milele ijayo. Hakuna hata mmoja kati yao atakayetupwa katika moto wa milele. Mimi Mwenyewe nitamkinga kwa namna ya pekee kila mmoja wao saa ile ya kufa kwao.
Kiongozi: Tuziombee roho za wale wanaoiheshimu kwa namna ya pekee Huruma ya Mungu, na kwa njia hii huwa sura hai za Moyo wa Yesu ulio na Huruma nyingi.
Wote: Ee Yesu mwenye Huruma, mwenye Moyo ulio Huruma yenyewe, uzipokee ndani ya Moyo wako wenye Huruma sana, roho za watu wale wanaoiheshimu na kuitukuza kwa namna ya pekee Ukuu wa Huruma yako. Roho hizi hushinda kwa nguvu ya Mungu mwenyewe. Hukazana kihodari, hata katikati ya taabu na dhiki za kila aina, wakiitumainia tu Huruma Yako, na kwa kujiunga nawe, ee Yesu, huwabeba wanadamu wote mabegani mwako. Watu hawa hutamani kushiriki Msalaba wako kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Uzidi kuwafunika kwa Huruma yako daima na uwajalie fadhila za uvumilivu, udumifu na nguvu za kuyasubiri yote. Amina.
Baba yetu,……. Salamu Maria …….. Atukuzwe, ………..
Wote: Baba wa Milele, uzitazame kwa macho ya Huruma, roho wa watu wale ambao kwa juhudi na upendo wa pekee, huitukuza na kuiheshimu Huruma yako isiyo na mipaka, ambao wameingizwa ndani ya Moyo wa Yesu ulio na Huruma tele. Watu hawa ni kama Injili iliyo hai. Wanakutukuza kwa maneno na matendo yao, na kwa kukuiga Wewe, huwatendea watu wenzao kwa wema na huruma. Tunakuomba uwaonyeshe Huruma yako Kuu zaidi na zaidi, kadri ya tumaini lao kwako na kwa ahadi zako. Mwanao Yesu Kristu Mwenyewe atawaleta kama utukufu wake, tangu wakati huu wakiwa bado hapa duniani. Lakini hasa saa yao ya kufa. Amina.
SIKU YA NANE
Maneno ya Mwokozi: “Leo niletee roho za wale waliofungwa bado toharani, na uwazamishe ndani ya Bahari Kuu ya Huruma yangu. Humo, mafuriko ya Damu yangu, yazimishe miali ya motto mkubwa unaowachoma. Roho hizi zote hupendwa sana nami. Wako humo toharani kwa ajili ya kulipia Haki yangu waliyoikosa hapa duniani. Wewe una uwezo wa kuwapatia faraja. Chota rehema zote za Kanisa langu na uzitolee kwa ajili yao. Ungalijua tu ukali wa mateso yao, loo! Ungetolea daima sadaka za kiroho kwa ajili yao, na kulipa deni zima la Haki ya Mungu”.
Kiongozi: Tuwaombee marehemu wa toharani, wanaoilipia Haki ya Mungu, ili mtiririko wa Huruma wa Damu ya Yesu uweze kupunguza na kufupisha mateso yao.
Wote: Ee Yesu mwenye Huruma uliyesema, “Muwe na Huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na Huruma”. Uzitazame kwa Huruma roho zile zinazoteswa toharani, kwa kulipia deni la Haki ya Mungu waliyoikosea. Mtiririko ule wa Damu na Maji uliotoka kwa kasi Moyoni mwako, uzimishe miale ya moto mkali wa toharani, ili huko pia Huruma yako isifiwe na kuadhimishwa. Amina.
Baba yetu ……. Salamu Maria ……. Atukuzwe ………
Wote: Baba wa Milele, uzitazame kwa wema na huruma, roho zile zinazoteswa Toharani, wao pia wameingizwa ndani ya Moyo wa Mwanao Mpenzi Yesu, na uchungu wote ulioelemea Moyo na Roho yake, onyesha Huruma yako kwa roho zilizotiwa nguvuni na Haki yako. Uwatazame watu hao kwa njia ya Madonda yake Yesu Mwanao Mpenzi, kwa kuwa tunaamini kabisa kuwa wema na Huruma yako havina mwisho. Amina
SIKU YA TISA
Maneno ya Mwokozi: “Leo niletee roho za wale waliokwishaingia hali ya uvuguvugu, na uwazamishe katika kilindi cha Huruma yangu. Roho hizi huumiza sana Moyo wangu. Roho yangu iliteseka sana kwa kinyaa cha kutisha kule bustanini kwa sababu ya roho hizi vuguvugu. Ni wao waliosababisha nilie; Baba ikiwa ni mapenzi yako uniondolee mbali kikombe hiki nisikinywe. Kwa watu hawa, tumaini la mwisho lililowabakia ni kuikimbilia Huruma yangu tu basi”.
Kiongozi: Tuwaombee watu walio na hali ya uvuguvugu, hali ya hatari kwa wokovu, ambao walisababisha mateso makali sana kwa Yesu Kristu kule bustanini mwa mizeituni.
Wote: Ee Yesu mwenye Huruma nyingi, Wewe u Huruma yenyewe, Uzipokee roho vuguvugu ndani ya Moyo wako ulio na Huruma bila kiasi. Roho hizi ni kama mizoga iliyojaa na kunuka uvundo, uziingize katika moto wa upendo wako safi, zitakasike. Roho hizi zilikutia kinyaa kingi. Sasa uziwashe tena, na kwa Huruma yako, uzipe paji la Upendo Mtakatifu. Ee Yesu mwenye Huruma Kuu, tumia uwezo wako na uzipatie roho hizi bidii tena, kwani kwako hakuna kitu kisichowezekana, na kwa njia hii wapate kuitukuza daima Huruma Yako. Amina.
Baba yetu, Salamu Maria ………..Atukuzwe,
Wote: Baba wa Huruma, uzitazame kwa macho ya Huruma, roho zilizo vuguvugu, ambazo katika hali yao hiyo, wameingizwa ndani ya Moyo wa Mwanao Yesu, ulio kilindi cha Huruma. Ee Baba wa Huruma, tunakusihi kwa ajili ya mateso makali ya Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, uliyovumilia pale msalabani, kwa masaa matatu ukiwa katika hali ya umahututi ya uchungu, uziwezeshe hata roho hizi zipupie utukufu wako. Uijaze mioyo ya watu hawa upendo wa kweli, hivyo kwa Baraka takatifu, waweze kutenda matendo mengi ya huruma hapa duniani, na huko Mbinguni wafike kuitukuza Huruma yako Kuu kwa milele yote. Amina.