SALA YA MWAKA WA HURUMA YA MUNGU NA PAPA FRANCIS
Bwana Yesu Kristo,
umetufundisha kuwa watu wenye huruma kama alivyo Baba wa mbinguni, na umetuambia kwamba mtu yeyote anayekuona wewe amemwona Baba. Tuoneshe uso wako nasi tutaokoka.
Jicho lako lililosheheni upendo lilimwokoa Zakayo na Mathayo waliokuwa watumwa wa fedha; lilimwokoa mwanamke mzinzi na Magdalena aliyekita furaha yake kwa kiumbe; ulimfanya Petro aangue kilio baada ya usaliti; ukamhakikishia Paradiso, mwizi aliyetubu. Tuwezeshe kila mmoja wetu kusikiliza lile neno ulilomwambia mwanamke Msamaria: Kama ungetambua zawadi ya Mungu!
Wewe ni sura inayoonekana ya Baba asiyeonekana; sura ya Mungu anayejifunua kwa uweza, lakini zaidi kwa njia ya msamaha na huruma: liwezeshe Kanisa lako duniani kuwa sura yako inayoonekana; Bwana wake, Mfufuka anayeishi katika utukufu. Wewe ulipenda kwamba,hata watumishi wako ambao wamevikwa na udhaifu waweze kuwa na huruma ya haki kwa wale wanaoogelea katika ujinga na makosa: tunakuomba basi, kila mtu anayemkaribia kila mmoja wao ajisikie kukaribishwa, kupendwa na kusamehewa na Mungu.
Peleka Roho wako Mtakatifu na utuweke sisi wakfu ili Jubilei ya Huruma ya Mungu iwe ni mwaka wa neema ya Bwana na Kanisa ambalo limepyaishwa kwa ari kuu liweze kuwatangazia maskini Habari Njema, kuwahubiria wafungwa na wanaosetwa uhuru na vipofu kuona tena.
Tunakuomba haya kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa huruma, Wewe unayeishi na kutawala pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, milele na milele. Amina